Wednesday, 30 September 2015

IT BRIDGE YAWAFIKIA WANAFUNZI 60,000

JUMLA ya wanafunzi 60,000 katika shule 150 nchini wamepitiwa na mafunzo ya programu ya Bridge IT yenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kidijiti (digital technology) katika ufundishaji na ujifunzaji wa Hisabati,Sayansi na Stadi za Maisha.
Hayo yamsemwa na Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome kuzindua maonesho ya Tehama.

Alisema kutokana na mafanikio yaliyotokea sasa wanatanua wigo baada ya kuwezeshwa kifedha na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya elimu (Global Partnership For Education) kwa ajili ya kuendeleza teknolojia hiyo katika kujifunza na kufundisha katika shule za msingi na hasa darasa la awali la kwanza hadi la nne.

Aidha maonesho hayo yanayofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere yana lengo la kuonesha ubunifu ambao upo tayari kutumika kufanikisha mafunzo hayo.

Pia maonesho hayo yanatarajia kujadili na kuangalia mbinu za kielektroniki zitakazoweza kuendana na mazingira ya Tanzania katika ufundishaji na kujifunza kwa gharama nafuu.

Pia wanatarajia kuangalia utayari wa walimu na namna ya kuwabadilisha mtazamo ili waweze kufundisha na kufundishika.
“Lengo la serikali kupitia Wizara ya Elimu ni kupanua wigo wa elimu hasa elimu ya awali kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo itabadilisha ufundishaji kutoka kutumia vitabu vilivyopo katika mfumo wa ‘hard copy’ na kuwa katika mfumo wa sauti na picha au ‘soft copy’,” alisema Profesa Bhalalusesa.
Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eusella Bhalalusesa akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome kuzindua maonesho ya Tehama yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius  Nyerere jijini Dar es Salaam. 
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifuatilia kwa makini risala Kamishina wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho ya Tehama yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo serikali imesema inatarajia kuanza kutumia rasmi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kufundishia wanafunzi kuanzia ngazi ya chini kabisa ya elimu ambayo ni chekechea.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema matumizi ya Tehama katika ufundishaji wa wanafunzi wa chekechea yataimarisha kiwango cha elimu.
“Dunia imebadilika sana hasa katika sekta ya elimu na mawasiliano, hatuna budi kuendana nayo kwa kasi ileile ya ukuaji wake kwa kuimarisha mifumo yetu ya ufundishaji,” alisema Profesa Mchome.
Alisema wizara yake imeanzisha mpango maalum utakaosaidia wanafunzi kujifunza kwa njia ya kisasa ya kutumia mbinu za kielektroniki katika kujifunza na hivyo kuimarisha uelewa na kuongeza hamasa ya ufundishaji kwa wanafunzi.
Profesa Mchome alisema maonesho hayo yana lengo la kupata wadau mbalimbali waliobuni programu zinazoweza kutumika katika kufundishia kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na hivyo watachaguliwa wachache wenye sifa na watakowezesha mafunzo hayo katika shule za Msingi na baadae katika ngazi ya sekondari.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akijianda kuzindua rasmi maonesho ya Tehama yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi jijini Dar walioshiriki hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shule Direct, Faraja Nyalandu akipozi na wadau kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam yanakoendelea maonesho ya TEHAMA.

 

No comments:

Post a Comment