WANAFUNZI WA ST. JOSEPH WACHANGIA CHUPA 125 ZA DAMU MUHIMBILI
Balozi
wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya akiwa na wanafunzi
wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa. Kutoka kulia ni Benjamin Fred,
Maria Joseph na Vanessa Elieza Mwakila.
Mmoja
wa wanafunzi akichangia damu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuokoa
maisha ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH)
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya akitoa damu leo jijini Dar es Salaam katika shule ya St.
Joseph Cathedral High School zamani ikijulikana Shule ya Sekondari
Forodhani. Balozi Msuya ambaye alisoma kwenye shule hiyo mwaka 1975 ni
mmoja wa wanafunzi wa zamani waliojitokeza kutoa damu ili kuokoa maisha
ya wagonjwa wanaotibiwa Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
WANAFUNZI
waliosoma St. Joseph Cathedral High School zamani ikijulikana Shule ya
Sekondari Forodhani leo wamejitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya
Watanzania ambao wanahitaji damu.
Wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa kwa kushirikiana na wenzao wa zamani wamefanikiwa kutoa chupa 125 za damu.
Akizungumzia
katika uchangiaji wa damu shuleni hapo , Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
Aminiel Aligaesha amesema suala la damu ni changamoto kwani hospitali
hiyo inahitaji wastani damu wa chupa 100 kila siku na kwamba kwa siku
hivi sasa zinapatikana chupa 24 hadi 40.
Alifafanua kwamba hivi sasa hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa wastani wa chupa 60 za damu kwa siku.
Kutokana na hali hiyo amewaomba
Watanzania kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya
Watanzania kwani suala hilo linagusa maisha ya watu wote.
Ametaja makundi ambayo huitaji damu kwa haraka kuwa ni wagonjwa wa dharura, mama wajawazito, watoto na wagonjwa wa saratani.
Aligaesha amewashukuru
wanafunzi hao na wale wanaosoma hivi sasa kwenye shule hiyo kwa
kujitokeza kwa wingi kuchangia damu na kusisitiza kuwa kitendo
walichokifanya ni cha kuigwa.
Kwa upande wa wanajumuia
waliosoma shuleni hapo wamesema wameamua kujitokeza kuchangia damu ili
kuwahamasisha wanafunzi kuwa na utamaduni wa kujitolea katika jamii
jambao ambalo hivi sasa limefifia.
Aidha
kwa upande wa MNH imekuwa ikitoa matangazo mbalimbali ili Watanzania
wajitokeze kuchangia damu kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu kwenye
hospitali hiyo.
Katika
shughuli ya leo, Balozi Msuya alifika katika shule hiyo na kuchangia
damu kama walivyofanya wanafunzi wengine waliosoma hapo miaka 1950.
Balozi
huyo alisoma katika shule hiyo mwaka 1975, baadhi ya wanafunzi wengine
ni Mariam Zialora ambaye amesoma hapo 1964, Glen Dias mwaka 1954, Saada
Jaha mwaka 1970, Albertina Doarado mwaka 1968, Solomon Mihayo mwaka
1990, Tahir Othman 1990, Edith Mabena mwaka 1992, Edward Makwani mwaka
1970 na Ephrahim Tumwidike mwaka 2012.
Leo
wanafunzi hao wa zamani wameonyesha upendo wa hali ya juu kuungana na
wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hivi sasa katika kuchangia damu.
Uamuzi huo wa wanafunzi hao wa zamani unapaswa kuigwa na shule nyingine
kwa lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.
Shughuli
ya kuchangia damu leo imefanywa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa
kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).
No comments:
Post a Comment