ELIMU YA STADI ZA MAISHA KUOKOA KUNDI KUBWA LA VIJANA WALIO NJE YA SHULE
Afisa
vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw.
Godfrey Massawe (aliyesimama) akifuatilia majadiliano ya wawezeshaji
kitaifa wakati wa kazi za kikundi kwenye Mafunzo ya Uwezeshaji wa Stadi
za Maisha yaliyofanyika Kanda ya Ziwa.
ILIGUNDULIKA
kuwa ulimwenguni kote na hususan nchini Tanzania, Vijana walio nje ya
shule ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari ya magonjwa
yanayoenea kwa njia ya ngono, VVU na UKIMWI kwa kutokuwa na taarifa na
stadi za kuwaongoza hivyo kupoteza kundi kubwa la vijana ambalo ni taifa
la kesho.
Ufumbuzi
wa tatizo hili umeweza kufanyika kwa kuwapa vijana stadi za maisha
zenye upeo mpana wa maarifa na stadi zinazoweza kuwasaidia vijana
kuendana na mazingira shindani yanayobadilika.
Stadi
za maisha ni moja kati ya mikakati iliyobainika kuleta mabadiliko ya
tabia za mtu. Stadi hizi uhusisha stadi na uwezo wa kujenga tabia njema
ili kuepukana na matatizo yaliyopo katika maisha ya kila siku.
Mkabala
wa stadi za maisha unalenga katika kuendeleza na kukuza stadi
zinazoitajika katika mahitaji ya maisha ya kila siku kama vile
mawasiliano, kufanya maamuzi, fikra, kuhimili mihemko, uthubutu, ujenzi
wa kujiamini, kuzuia shinikizo rika pamoja na mahusiano.
Mkabala
huu pia unashughulikia ukuaji wa mtu ili awe na stadi za kumwezesha
kutumia aina zote za taarifa kuhusiana na masuala kama vile magonjwa ya
ngono, VVU na UKIMWI.
Mahitaji
ya stadi za maisha miongoni mwa vijana ni mengi na yanatofautiana baina
ya vijana wadogo na wakubwa, vijana walio nje ya shule na walio
shuleni, pamoja na walio na wasio katika ndoa hivyo kupelekea kuwa na
viwango vya mafunzo ya stadi za maisha vilivyopendekezwa na kubuniwa
kuwanufaisha vijana wasio mashuleni.
Wizara
inayosimamia masuala ya vijana imekua ikitoa mafunzo ya stadi za maisha
kwa vijana walio nje ya shule ili kuwapa vijana stadi za kukabiliana na
changamoto za kila siku katika maisha yanayowazunguka.
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na shirika la
umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA)
wameweza kufikisha elimu ya stadi za maisha kwa wawezeshaji wa kitaifa
kutoka kanda ya Ziwa hivi karibuni ili kuweza kusambaza elimu hiyo kwa
vijana walio nje ya shule maeneo yote ya kanda ya ziwa hivyo kuwawezesha
vijana kukabiliana na dunia hii ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Akifungua
mafunzo ya wawezeshaji kitaifa kutoka kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoa
wa Mwanza hivi karibuni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo Bibi. Sihaba Nkinga aliwataka wawezeshaji kitaifa wa stadi za
maisha kuwasaidia vijana kujitoa katika mitazamo hasi na kuleta
mabadiliko chanya katika jamii kwani vijana ndio nguvu kazi ya Taifa
hili.
“Vijana
wakijiimarisha katika shughuli za kijamii na kiuchumi wataepuka
kuzungukwa na vihatarishi vya maisha kama vile VVU na Ukimwi, mimba
zisizotarajiwa pamoja na dawa za kulevya hivyo kujenga nchi kwa kutumia
nguvu kazi ya vijana” alisema Bibi. Nkinga.
Mafunzo
ya stadi za maisha yamekua yakiongeza hali ya kujiamini kwa vijana na
kutoa mbinu za kukabiliana na matatizo ya maisha kwa kuwapa vijana uwezo
wa kutumia muda wao kikamilifu kuzungumza na watu wasiowajua kuliko
ilivyokua hapo awali.
Aidha
Bibi. Nkinga alisema kuwa matarajio ya serikali ni kuona vijana wa
kitanzania wanajitambua kua wao ni nani, wanaenda wapi, na watafikaje
kwa kujua uwezo na udhaifu binafsi walionao ili waweze kupanga malengo
waliyonayo na kuyatekeleza kulingana na fursa zilizopo.
Vijana
wanaopata fursa ya kuwezeshwa katika stadi za maisha wameongeza viwango
vyao vya stadi za kujitambua na uwezo wa kuwasiliana na watu wa rika
zote hivyo kubadili tabia za vijana wa rika mbalimbali.
Mkurugenzi
Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bw. James Kajugusi amesema kuwa kila kijana ana sifa za kujiunga
na mafunzo ya stadi za maisha zitakazowawezesha kukataa visingizio kama
vile umasikini, maradhi na masuala yanayoshauriwa na marafiki ambayo
yanaweza kuwaingiza katika vishawishi.
Bw.
Kajugusi amesema kuwa Mafunzo ya stadi za maisha yamelenga kupata
waelimishaji wa kitaifa wa stadi za maisha watatu kutoka kila mkoa
katika mikoa yote ya Tanzania bara ambao watawafikia waelimishaji rika
wa kila mkoa ili kuweza kufikisha elimu waliyoipata kwa vijana wa rika
mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, kata, vijiji, vitongoji, mitaa, vijiwe
na sehemu rasmi za shughuli za vijana.
Stadi
za maisha zinaweza kuwekwa katika makundi matatu ambayo ni stadi za
maisha kwa ajili ya kujitambua, kwa ajili ya fikra na kwa ajili ya
mahusiano baina ya watu hivyo kwa pamoja aina hizi huweza kutoa majibu
kwa vijana kuwa wao ni nani, wanataka kwenda wapi na watafikaje hapo
wanapotaka kwenda.
Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bibi. Susan Ndunguru amesema kuwa vijana
waliopata mafunzo ya uwezeshaji wa stadi za maisha ni mabalozi ambao
kama watatumia vizuri uwezo walioupata katika mafunzo hayo watabadili
fikra za vijana wengi nchini hivyo kuweza kujenga taifa lenye afya
nzuri, weledi pamoja na ujuzi.
Stadi
za maisha humjenga kijana kufanya maamuzi sahihi hivyo kuondokana na
majuto na kumfanya kuwa huru katika kutoa maamuzi binafsi.
Kwa
kawaida stadi za maisha humpa kijana mwitikio wa uthubutu unaompa fursa
ya kusimamia anachotaka au anachoamini bila kumdharau au kuumiza
kihisia mtu mwingine.
Mtaalamu
wa masuala ya Stadi za Maisha Bw. Benny Lugoe amesema kuwa wawezeshaji
wa kitaifa waliopata Mafunzo ya Stadi za Maisha wana ari na motisha ya
kujifunza na kama wataendelea kuwa na ari hiyo watakua wabunifu na
wawezeshaji wazuri kwa vijana ndani ya jamii wanazoishi.
Aidha
Mwezeshaji wa Kitaifa wa Stadi za Maisha kutoka Mkoa wa Shinyanga Bw.
Ezra Manjerenga amesema kuwa vijana wa Mkoa wa Shinyanga wamekua
wakikabiliwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi hivyo ugeni wa mafunzo
ya stadi za maisha katika Mkoa huo utawavutia vijana wengi jambo ambalo
litapelekea kutimiza lengo la serikali kufikisha mafunzo hayo kwa
vijana wa rika mbalimbali.
Stadi
za maisha zinatoa fursa kwa vijana kupata taarifa za afya ya uzazi na
upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi, pia humpa kijana haki ya
kutambuliwa, kusikilizwa na kuheshimiwa utu wake bila kujali kiwango cha
elimu, hadhi yake au sifa nyingine itakayombagua na kumuweka katika
mazingira hatarishi.
Vijana
waliopata mafunzo ya stadi za maisha wamepewa dhamana na serikali
kwenda kuwatumikia vijana na kuhakikisha kuwa uhamasishaji wa mabadiliko
chanya miongoni mwao ili kuweza kuachana na tabia zote hatarishi na
kushiriki vyema kwenye shughuli za uzalishaji mali.
Serikali
inatambua kuwa vijana ni rasilimali muhimu kwa ajili ya ukuaji wa
uchumi na kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwa ujumla hivyo kusimamia kwa
ukaribu zaidi elimu ya stadi za maisha kwa vijana wote nchini.
No comments:
Post a Comment