Monday, 14 March 2016

KAMPUNI YA G4S NA TAASISI YA BHUBESI PRIDE FOUNDATION WAUNGANA KUINUA MCHEZO WA RAGA NA KUJENGA UWEZO KWA WANAFUNZI WA KITANZANIA

Mkuu wa Mauzo na Masoko wa kampuni ya G4S, Alfred Elia, (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2016 kuhusu ushirikiano baina ya kampuni yake na taasisi ya kujitolea ya Uingereza ya Bhubesi Pride Foundation, (BPF), ambapo taasisi hiyo inaendesha mafunzo ya kuunyanyua mchezo wa Raga (Rugby), pamoja na  kusaidia jamii pamoja na maendeleo mashuleni na kwenye vituo vya kijamii. Shule sita sita za jijini Dar es Salaam zitashindana katika mchezo huo Jumamosi hii jijini. Wengine pichani, ni Meneja mradi wa BPF, Mark Cole, (kulia) na Mkuu wa masuala ya fedha wa G4S, Paul Fullers.Mkutano huo na waandishi wa habari ulifanyika jana Machi 14, 2016


Finn Sims, Meneja anayehusika na vyombo vya habari wa BPF


Mark Cole, Meneja mradi wa BPF


 Paul Fullers, Mkuu wa masuala ya fedha wa G4S
 
TAASISI ya kujitolea ya Uingereza ya Bhubesi Pride Foundation (BPF) kwa kushirikiana na kampuni ya ulinzi ya G4S ya jijini Dar es Salaam, inaendesha mpango wa kuunyanyua na kuuendeleza mchezo wa Raga, (Rugby), kusaidia jamii pamoja na maendeleo mashuleni na kwenye vituo vya kijamii.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya G4S barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2016, Mkuu wa kitengo cha Mauzo na Masoko cha G4S, Alfred Elia, amesema, tayari mafunzo hayo yamefanyika jijini Arusha na sasa yako hapa jijini Dar es Salaam na yameanza rasminleo Jumatatu Machi 14, 2016 ambapo jumla ya shule sita za msingi ziko kwenye mpango huo.
Amezitaja shule hizo kuwa ni pamoja na shule ya msingi, Mapambano, Makumbusho, Hananasifu, Victoria, Mugabe na Shekilango.
Kwa upande wake, Meneja wa BPF, Mark Cole, alisema, mpango huo unaendeshwa kwenye nchi mbalimbai za Afrika na ni wa mwaka mmoja. “Tayari tumefanya mafunzo haya nchini Uganda, Kenya, Tanzania, Msumbiji, Malawi, Zambia, Botswana, Namibia na Afrika Kusini, alisema Cole
Alisema, nia ya mpango huo ni kuunganisha jamii kupitia raga, kuelimisha thamani na stadi za maisha, pamoja na kunyanyua uwezo wa walimu nchini, kulea viongozi wa jamii, wake kwa waume pamoja na kuweka uwezeshaji huu kuwa endelevu.
Maendeleo ya matokeo ya muda mrefu kupitia miradi inayoonekana, mfano kupanda miti, kwa kushirikiana na wabia wetu katika nchi tajwa.
Tayari shirika hili kwa kushirikiana na G4S Tanzania limeishafanya haya Arusha na Moshi ambapo watoto zaidi ya watoto 600 wa mikoa hio walipata mafunzo ya raga pamoja na stadi za maisha ambapo pia G4S ilipanda miti katika maeneno mbalimbali
Naye Mkuu wa masuala ya fedha wa G4S, Paul Fullers, alisema, G4S kwa kutambua masuala ya usalama, ndio maana imeamua kushirikiana na BPF ili kujenga uelewa miongoni mwa wanafunzi kuhusu masuala ya usalama wawapo shuleni, mabarabarani na hata nyumbani.
“Mafundisho haya yanafanyika kila mwaka kuanzia mwezi January mpaka Julai, ambapo shuguli za kijamii hufanyika sambamba na makampuni yanayojitolea kudhamini- G4S Africa, akiwa ni mdhamini mkuu na muhimu kwa hii taasisi.” Alifafanua Fullers.
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs). Vyama vya raga kitaifa, idara mbalimbali za kiserikali, shule za kimataifa pamoja na makampuni mbalimbali kwenye jamii husika, kuongezea thamani katika huu uhusiano pamoja na kujengea uwezo, alisema.

SHULE YA MSINGI MBAGALA MAJIMATITU YACHIMBIWA VISIMA VYA MAJI.

 Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela akiangalia maendeleo ya kisima kimoja kati ya viwili vinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.

 Wataalam kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) wakiendelea kuchimba kisima chenye urefu wa mita 130 katika shule ya Msingi Mbagala majimatitu, Temeke jijini Dar es salaam.

 
Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela na Mhandisi Elizabeth Kingu, Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Maji (kushoto) wakiangalia maendeleo ya moja ya kisima kinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
 
Walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Majimatitu iliyoko Temeke jijini Dar es salaam watanufaika na huduma ya maji safi kufuatia Serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 24.5 kwa lengo la kufanikisha mradi wa uchimbaji wa visima viwili kwa lengo la kuboresha taaluma na mazingira ya shule hiyo.

Akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo leo jijini Dar es salaam msimamizi wa mradi huo kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Abel Chibelela amesema kuwa kuchimbwa kwa visima hivyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali kuitaka DAWASA kutafuta vyanzo vya maji katika shule hiyo ili kuwaondolea adha ya uhaba wa Maji.



Amesema shule hiyo imekuwa na tatizo hilo kufuatia kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 6000 inayozidi uwezo wa miundombinu iliyopo sasa ikiwemo kisima kinachotumiwa na wanafunzi hao kinachozalisha lita 8000 kwa siku wakati mahitaji halisi ya maji ni Lita 40,000 kwa siku.

 

Amesema Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa ( DDCA) ilipewa jukumu la kuchimba visima viwili  vya shule hiyo kwa thamani ya shilingi milioni 24.5 zikiwa ni gharama za uchimbaji, usafishaji wa visima hivyo na gharama za vipimo vya maabara ili kuangalia ubora wa maji hayo.

 

" Kazi ya uchimbaji wa visima hivi vyenye urefu wa mita 130 na 140 imeanza rasmi na itachukua siku 14, tunafanya haraka ili tuweze kujua wingi wa maji yaliyopo na ubora wake kama inafaa kwa matumizi ya binadamu"
 
Pia amesema DAWASA itasimamia ujenzi wa minara mirefu ya matenki na kuongeza matenki makubwa yatakayokidhi mahitaji ya shule hiyo yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 20 kwa kila shule.
Kwa upande wake Mtaalamu kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kuchimba visima hivyo na DAWASA Bw. Nungwe Gwaga akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo amesema kuwa wao kama wataalam wa kuchimba visima walifanya utafiti katika eneo hilo na kujiridhisha kuwa eneo la shule ya Msingi Mbagala Maji Matitu lina Maji ya kutosha.
 
" Sisi kama wataalam tulifanya utafiti (Physical Survey) katika eneo hili ili kujua kama kuna maji na miamba inayopita pale pamoja na umbali wake, sisi tumejiridhisha tutachimba mita 130 ambazo tayari zimetupa majibu ya kuwepo kwa Maji "
 
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw. Abdul Mgomi akifafanua kuhusu visima hivyo amesema vitawezesha shule yake kuondokana na adha ya uhaba wa huduma ya maji inayowakabili wanafunzi shuleni hapo kufuatia mwitikio wa wazazi kuwaandikisha watoto wao shuleni hapo kwa mwaka 2016.
 
Amesema kwa sasa shule hiyo inatumia kisima kidogo chenye uwezo wa kuzalisha lita 8000 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji halisi ya lita 32000 kwa wanafunzi 6000 wanaosoma shuleni hapo.
 
Mwalimu Mgomi ameshukuru jitihada zilizofanywa na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo Mhe. Said Mecki Sadiki kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuchimbia visima hivyo.
Ameeleza kuwa mara baada ya visima hivyo kukamilika  uongozi wa shule utaweka utaratibu wa matumizi ya maji hayo kwa shule na ziada itakayopatikana na maji itauzwa kwa majirani wanaoishi kuzunguka shule hiyo ili mradi uweze kujiendesha wenyewe.
 
Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa kujenga mapya 10 ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi 6000 waliopo shuleni hapo pamoja na ujenzi wa shule nyingine 2 zitakazoondoa kabisa tatizo la mrundikano wa wanafunzi.
 
Naye mmoja wa Wazazi na Mjumbe wa Kamati ya Miradi ya shule hiyo Bi.Happiness Mgulambwa akizungumza katika eneo vinapochimbwa visima hivyo ameishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha wazazi na wanafunzi hao kwa kuamua kuwachimbia visima hivyo huku akiongeza  kuwa upatikanaji wa huduma ya maji shuleni hapo utaongeza ufanisi kwa walimu na wanafunzi.
 
Amesema wao kama Wazazi kupitia kamati ya miradi ya shule hiyo waliiomba Serikali kuwasaidia kupata maji kwa wanafunzi shule hiyo  ili kuondoa kero ya maji jambo ambalo lilikubaliwa.
 
" Kweli wanafunzi wa shule hii walikua wanapata shida,uhaba wa maji hapa shuleni uliwalazimu kuja na maji kwenye madumu jambo liliowafanya wakati mwingine kufika wamechoka na hata kuchafuka, tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya tano kwa kutusaidia" Amesema Bi.Mgulambwa.

 
 
 


Sunday, 21 February 2016

TPB YAKABIDHI SHULE VYOO VYA THAMANI YA TSH.MILIONI 4.7

 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua vyoo vyenye matundu 14, vitakavyohudumia wanafunzi 850 katika shule ya Msingi ya Makambi, Songea Mkoa wa Ruvuma, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 4.7 kulia ni Meneja wa Oparesheni wa tawi la Songea, Simon Mlelwa 
Wanafuzni wakishangilia kupata vyoo
 
 Sehemuya vyoo hivyo

 Wanafunzi wa shule ya msingi ya Makambi iliyopo Kata ya NdilimaLitembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakifurahia vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Benki ya Posta Tanzania. 

BENKI ya posta Tanzania, TPB, imekabidhi vyoo vyenye thamani ya shilingi milioni 4.7 kwa shule ya msingi Makambi iliyoko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akikabidhi vyoo hivyo vyenye matundu 14 vilivyojengwa na benki hiyo ili kusaidia kuondokana na upungufu wa vyoo kwenye shule hiyo mwishoni mwa wiki, Meneja mahusiano na mawasiliano wa TPB, Noves Moses, alisema msaada huu wa benki nisehemu ya mchango kwa jamii katika kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kufikia lengo la kutoa elimu bora hapa nchini.
Kwa kutambua juhudi za Rais za kutoa elimu bure kwa wanafunzi kote nchini, ambapo kumekuwepo na ongezeko kubwa sana la wanafunzi, benki ya posta inayofuraha kuunga mkono juhudi za Mh.Rais na msaada huu wa vyoo utasaidia kuweka mazingira bora ya utoaji elimu lakini pia mahudhurio ya wanafunzi, alisema Noves.
Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wadau wa elimu kulichukulia suala la elimu bure kama kigezo cha kutokuchangia sekta hiyo na baadala yake wanadai ni kazi ya serikali pekee jambo ambalo siyo sahihi katika uboreshaji elimu.
 
“Suala la elimu bure lisiwe kigezo cha wadau kushindwa kuichangia sekta hiyo kwani kufanya hivyo kunapelekea baadhi ya shule kushindwa kuwa na mazingira mazuri ya watoto kujisomea pamoja na walimu wao kutokuwa na morali ya kufundisha” alisemaMeneja huyo wa mahusiano na mawasiliano.
Noves alisema kuwa Benki ya Posta Tanzania inafanya kazi kwa kiwango kikubwa na serikali hivyo imetoa misaada mbalimbali ya kijamii hasa kwa upande wa afya na elimu huku katika upande wa elimu wamechangia madawati na ujenzi wa vyoo bora vya kisasa kwenye shule mbalimbali hapa nchini .
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Kanisius Ngongi awali akitoa taarifa ya shule hiyo kabla ya kukabidhiwa vyoo hivyo alisema kuwa shule hiyo inawanafunzi 850 na matundu ya vyoo yapo 14 na kuwa vyoo vyote vina maji ya kutosha.
Ngongi aliipongeza benki hiyo alisema kuwa shule hiyo kwa sasa imeshabadilika,mazingira yamekuwa bora kwa upande wa vyoo vya wanafunzi ambavyo kwa sasa hakuna shule ndani ya Manispaa hiyo yenye vyoo kama hivyo.
Mwalimu Ngongi alisema kuwa licha ya vyoo vya wanafunzi kuwa bora lakini bado kunachangamoto ya vyoo vya walimu maana vyoo walivyokuwa wakivitumia vimeshapoteza ubora wake na kuwafanya walimu hao kupata shida mahala pa kujisitili hivyo amewaomba wadau mbalimbali waweze kuchangia kama Benki ya Postainavyojitolea.